May 29, 2013

DK. CHENI ALISHWA SUMU


Na Mwaija Salum
MWIGIZAJI mwenye ushawishi mkubwa Bongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ ameponea chupuchupu kwenye hatari ya kupoteza maisha baada ya kula chakula kilichosadikika kuwa kina sumu, Risasi Mchanganyiko linaripoti.
Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ akiwa hoi hospitalini.

Habari kutoka kwa chanzo chetu kilicho karibu na Dk. Cheni zinasema kwamba, msanii huyo ambaye pia ni mshehereshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii, alipatwa na mkasa huo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kutoka kwenye shughuli aliyokuwa akiiongoza kama Mc, Mwenge, Dar.

CHANZO KINATIRIRIKA


“Siku hiyo Dk. Cheni alikuwa kwenye sherehe maeneo ya Mwenge. Shughuli ilipoisha akaamua kwenda nyumbani kwake lakini akiwa njiani akaanza kuhisi maumivu makali ya tumbo.


“Alipofika nyumbani aliamua kunywa maziwa ili kusafisha tumbo, ikawa kama ndiyo amejizidishia maumivu. Asubuhi yake akaamua kwenda katika Hospitali ya Burhan ili apate tiba. Baada ya vipimo ikagundulika kuwa alikula chakula chenye sumu.


“Jamaa amelazwa pale na kutokana na hali yake ilivyo, ilibidi awekwe chini ya uangalizi maalumu wa madaktari ili sumu iweze kuondolewa mwilini.”
Dk. Cheni na mkewe wakiwa hospitalini. DR CHENI ASEMA HAYA!!!

“Unajua siku hiyo nilikuwa kwenye shughuli pale Mwenge, wakati wa chakula nilikuwa nakula huku nikiendelea na kazi kwa hiyo kuna wakati niliacha sahani yangu mezani. Kama kuna mtu aliamua kunifanyia hivyo, nadhani alitumia ule muda ambao nilikuwa nasimamasimama,”
alisema Dk. Cheni na kuongeza:


“Lakini namshukuru Mungu, madaktari wamenihakikishia nitakuwa sawa. Sasa hivi wanafanya kazi ya kutoa sumu mwilini kwa kutumia dozi maalumu ya vidonge na dripu kama unavyoona ila nina haueni kidogo, ukilinganisha na nilivyofikishwa hapa na mke wangu.”
...Akisikilizia dripu.

Alipoulizwa ni kwa nini anaamini kuwa sumu hiyo iliwekwa kwenye chakula alipokuwa kwenye sherehe alisema: “Ukweli ni kwamba chakula cha mwisho kabla ya kuanza kuhisi maumivu ya tumbo nilikula pale. Sanasana baadaye nilikunywa maziwa kabla ya kuzidiwa na kuletwa hapa.”


POLE DK. CHENI
Timu ya gazeti hili inatambua umuhimu wako katika kupambana na maisha kwenye jamii. Tunajua kuugua kwako kumekwamisha mambo yako mengi lakini usijali ni mapito tu. Tunakutakia afya njema na upone haraka. Pole sana Dk. Cheni. – Mhariri.