Jun 3, 2013

KAMATI YA NGWEA YAKUSANYA MILIONI 32....MAMA MZAZI APANDWA NA PRESHA BAADA


kamati ya Mazishi ya aliyekuwa Msanii wa Bongo Fleva, Albert Mangwea ‘Ngwea’, mpaka jana mchana ilikuwa imekusanya jumla ya Sh milioni 32 kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kamati hiyo inahitaji Sh milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini mpaka Morogoro kwa ajili ya mazishi. Fedha hizo pia zinahitajika kwa ajili ya kuratibu shughuli nzima ya mazishi.

Mangwea alifariki dunia Jumanne iliyopita nchini Afrika Kusini akiwa usingizini kwa madai ya kuzidisha matumizi ya madawa ya kulevya.

Alitarajiwa kuwasili nchini jana lakini kushindwa kutoka kwa ripoti ya uchunguzi wa madaktari kwa wakati, kumesababisha isijulikane atatua lini, licha ya kudaiwa kuwa anaweza kutua leo.

Kamati ya Mazishi bado inaendelea na mchakato wa kuratibu shughuli hiyo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na mwandishi wetu akiwa Mbezi Goig jijini Dar ambako ndiko kwenye msiba huo, mmoja wa waweka hazina wa kamati hiyo, Paul Matthysse ‘P-Funk’, alisema mpaka sasa kamati yake imefikisha Sh 32,259,000 ingawa wanatarajia kuendelea kupokea michango mbalimbali kutoka kwa wadau.

Miongoni mwa watu wa kwanza kutoa michango yao katika msiba huo ni P-Funk aliyetoa Sh milioni tano, Clouds Media Group (Sh milioni tano) na Push Mobile (Sh milioni tano).

Juzi Kampuni ya Global Publishers ilitoa Sh milioni moja.
“Nawasisitiza Watanzania waendelee kutoa michango yao kwa ndugu yao ili kuonyesha umoja tulionao. Fedha zikiwa nyingi tunataka kumfanyia kitu mama yake ili kuendelea kumfariji kwani kipindi hiki ni kigumu kwake,” alisema P-Funk.

Wakati huohuo jana taarifa zilisema mama mzazi wa Mangwea aishie Morogoro, Denisia Mangwea, alipandwa na presha baada ya jana kupata taarifa kuwa mwili wa mwanaye umezuiwa Afrika Kusini kutokana na uchunguzi wa madawa ya kulevya. Alikimbizwa hospitali na inadaiwa anaendelea vizuri.

Mangwea aliwahi kutamba na nyimbo kadhaa kali zikiwemo Gheto Langu, She Got a Gwan, Mikasi na Tupo Juu.

YA MWILI WA NGWEA KUZUIWA HUKO AFRIKA KUSINI