Jun 25, 2014

BAADA YA KUTOLEWA KWENYE FAINALI ZA KOMBE LA DUNIA KOCHA WA ITALIA AJIUZULU

Baada ya kutolewa kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka huu huko nchini Brazil kwa kufungwa bao moja kwa sifuri na timu ya taifa ya Uruguay, Cesare Prandelli ametangaza kujiuzulu nafasi ya ukocha wa timu ya taifa ya Italia.


Prandelli, amesema maamuzi ya kujiuzulu aliyachukua mara baada ya mchezo dhidi ya Uruguay ulipomalizika jana jioni kwa saa za hapa nyumbani, ambapo amekiri kumfikishia salamu hizo raisi wa chama cha soka nchini Italia Giancarlo Abete.


Kocha huyo ambae alikichukua kikosi cha Italia mara baada ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 zilizounguruma nchini Afrikla kusini, amesema alikuwa hana budi kuchukua maamuzi ya kujiuzulu kutokana na kushindwa kufikia lengo alilokuwa amejiwekea.


Amesema anaamini alipoiacha timu ya taifa ya Italia si pabaya sana, hivyo kocha ajaye ataendeleza mazuri ambayo atayakuta na hatimae kufikia malengo yanayotarajiwa na mashabiki wa soka nchini humo.


Hata hivyo amekanusha taarifa za kushurutishwa na mtu yoyote kuchukua maamuzi hayo, na amewataka mashabiki wa soka nchini Italia kutambua kwamba amefanya hivyo kwa maslahi ya taifa lake.

0 comments:

Post a Comment