Jun 23, 2014

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (Cuhas), mkoani Mwanza ATEKWA NA KULEWESHWA MADAWA JIJINI MWANZA

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Bugando (Cuhas), mkoani Mwanza, Musa Mdede, ambaye inadaiwa kuwa alitekwa nyara amepatikana akiwa hajitambui na mwenye uchomvu mwingi.

Mdede alirejeshwa kwenye nyumba alikokuwa amepanga akiwa hoi huku akionekana kuchoka akiwa hatambui alichotendewa wala waliomtendea.

Mdede ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), alitoweka Juni 18, mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha, muda mfupi wakati akijiandaa kwenda kurudisha fomu za kuomba kutetea nafasi yake katika uchaguzi wa viongozi wa serikali hiyo.

Waziri Mkuu wa serikali ya wanafunzi wa Cuhas, Benjamini Thomas, alisema Mdede alifikishwa kwenye nyumba alikopanga eneo la Nyakato na kukabidhiwa kwa mama mwenye nyumba juzi saa tano asubuhi na watu waliojitambulisha ni wasamaria wema.

“Kwa mujibu wa mama mwenye nyumba, walifika vijana wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka 30, walijitambulisha ni wafanyabiashara na kueleza kuwa walimuokota kijiji cha Usagara wilaya ya Misugwi na kumuhifadhi nyumbani kwao eneo la Igoma,” alieleza.

Alisema: “Walimuuliza mama mwenye nyumba kama anamtambua kijana huyo na alivyokubali walimuacha na kuahidi kurudi jana saa tano kumuona, lakini hadi sasa hawajarudi.”

Thomas alisema mama huyo alimuuliza Mdede ni kina nani angewapatia taarifa za kupatikana kwake na kutaja kaka yake ambaye ni mfanyakazi wa benki ambaye alifika saa nane mchana.

Alisema baada ya kufika aliwajulisha viongozi wa wanafunzi wa Cuhas na walipokwenda kumuona Mdede alikuwa bado katika hali mbaya.

“Alitutambua, lakini hakuweza kueleza lolote lililotokea tangu siku aliyochukuliwa, alichofanyiwa na wala alikokuwa, zaidi alieleza kuwa amechoka sana na anahitaji muda mwingi wa kupumzika,” alisema Thomas.

Waziri Mkuu huyo alisema walimpeleka hospitali ya Rufaa Bugando na kufanyiwa uchunguzi na madaktari kueleza kuwa hana tatizo lolote na kumruhusu kwenda nyumbani kupumzika.

“Kwa sasa amepumzika eneo la tofauti na alikokuwa akiishi, hiyo ni kwa ajili ya usalama wake, pia yupo chini ya uangalizi wa Polisi,” alisema Thomas.

Thomas alisema baada ya kupatikana na polisi kujulishwa, walitaka wanafunzi kumchukua bila kufanyiwa uchunguzi wowote, lakini waligoma na kutaka hadi atakapofanyiwa uchunguzi wa kina wa daktari.

“Kwa hali aliyokuwa nayo inaelekea alinywesha dawa siyo ulevi wa kawaida hadi mtu apoteze fahamu, ndiyo mana tumetaka uchunguzi wa daktari ambao wamemfanyia uchunguzi wa awali na kuchukua vipimo vingine ambavyo majibu yake bado,” alisema Thomas.

Alisema tukio hilo linawapa shaka kubwa kwa kuwa haijulikani waliomkamata, walikokuwa wamemuweka na hadi kumrudisha eneo alilokuwa akiishi.

“Usalama wa viongozi na wanafunzi uko shakani wakati wote…tunalitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuanzia kupotea kwake kunahusishwa na nini na taarifa itolewe kwa umma,” alisema Thomas na kuongeza:

“Tunataka kujua alipoteaje, alikuwa anafanywa nini, amepatikanaje.”

Alisema baada ya hali yake kutengamaa wataitisha mkutano na waandishi wa habari kuona kama anaweza kueleza alikokuwa na yaliyomsibu akiwa huko.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola, alithibitisha kupatikana kwa Mdede na kusema alipatikana kutokana na ushirikiano wa wasamaria wema na Jeshi la Polisi. Aliongeza kuwa aliokotwa akiwa katika hali ya ulevi, bila kueleza ni wa aina gani.

“Alipatikana akiwa hajitambui, akiwa kama amelewa, tunaendelea kumuhoji,” alisema.

Hata hivyo, alipotakiwa kufafanua zaidi alisema yupo kwenye msafara wa Makamu wa Rais na kwamba taarifa alizotoa zinatosha na hataweza kutoa taarifa zaidi ya hizo.

Kwa mujibu wa Thomas, Juni 18, mwaka huu, saa 10 hadi 12 jioni ulikuwa ndiyo muda wa mwisho kikanuni kurudisha fomu za kuwania nafasi ya uongozi katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu, huku Mdede alitarajiwa kupambana na wagombea wengine wawili.

Wakati wa kurudisha fomu watu wa karibu na mgombea mwenza wa Mdede, Moses Madenge, walipanga kurudisha fomu pamoja, lakini walimsubiri bila kutokea.

SIRI NYUMA YA PAZIA

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka chuoni hapo, enzi za uongozi wake Mdede aliwahi kuwaeleza kuwa alikuwa akipata mashinikizo kutoka kwa watu ambao hajawataja wakimtaka atoe tamko kuhusiana na mchakato wa Katiba mpya ya Tanzania.

Kutokana na tukio la kupotea kwa Mdede katika mazingira ya kutatanisha, juzi Spika wa Bunge la Wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DT), Yuda Gurty, alisema wanafunzi wa vyuo vikuu nchini walitarajia kufanya mgomo nchi nzima, kushinikiza Jeshi la Polisi kueleza alipo Mwenyekiti huyo.

Ingawa hadi sasa haijathibitika kuhusiana na chanzo cha tukio hilo, lakini kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, makundi kadhaa yamekuwa yakijipanga kivyama kutafuta kuungwa mkono katika vyuo vikuu.

Tahliso kama taasisi inayowaunganisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ina ushawishi mkubwa wa kisiasa na baadhi ya wanasiasa wanaotafuta nafasi kubwa za kisiasa wamekuwa wakiitumia kufanikisha malengo yao.

MFARAKANO TAHLISO

Akikabidhi madaraka kwa Musa Mdede mapema mwaka huu aliyekuwa Mwenyekiti wa Tahliso, Amon Chakushemeire, alituhumu kwamba wapo wanasiasa wanajipanga kuitumia kwa urais mwaka 2015.

Aliasa jumuiya hiyo iendelee kuendeshwa kitaaluma na si kisiasa.

“Wapo wanasiasa wanaotarajia kugombea urais mwaka 2015 wanaingilia uongozi wa Tahliso kwa utashi wao ili iendeshwe kisiasa, hali iliyosababisha kutaka kuingiza usiasa na kutuletea wagombea wao katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana,” alisema.

Chakushemeire alisema licha ya jumuiya hiyo kutegemea taasisi za nje katika kujiendesha, lakini katiba yao hairuhusu kushirikishwa wanasiasa ikiwamo kusaidiwa na taasisi zinazojiendesha kisiasa.

Alisema changamoto inayoikabili Tahliso ni wimbi la wanafunzi wa elimu ya juu kugubikwa na siasa badala ya kuweka malengo katika elimu itakayowanufaisha kwa maisha yao ya baadaye.

MATUKIO MENGINE YA UTEKAJI

Ukiacha tukio la kutoweka Mdede, yamewahi kutokea matukio kadhaa ya utekeji na utesaji wa baadhi ya viongozi wa taasisi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa usiku wa Juni 25 mwaka 2012 na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto ambao walimjeruhi vibaya ikiwemo kumng’oa meno na kucha.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, Mei 5, 2013 alivamiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, Jijini Dar es Salaam.

Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Limited ambayo ni wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African, katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kumkata kidole, kumjeruhi kwa kitu kizito kichwani na kumharibu jicho la kushoto.

Hadi leo hakuna mtuhumiwa yeyote ambaye amekamatwa na polisi kwa ukatili, mateso na hujuma walizotendewa Kibanda na Ulimboka.


CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment