Sep 6, 2014

Lampard: Chelsea Wangekuwa Tayari Ningebaki Stamford Bridge

Kiungo kutoka nchini Uingereza Frank James Lampard amesema angekuwa tayari kubaki na klabu ya Chelsea kwa kipindi kingine, endapo uongozi wa klabu hiyo ungekubali kumsainisha mkataba mpya.

Lampard ambaye kwa sasa anaitumikia kwa mkopo klabu bingwa nchini Uingereza Man City akitokea kwenye klabu ya New York City FC ya nchini Marekani, amesema lengo lake halikuwa baya na klabu ya Chelsea, lakini viongozi hawakumuonyesha kama wapo tayari kuendelea nae.

Amesema alikuwa anaamini bado nafasi ya kuitumikia Chelsea ilikuwepo na aliipenda sana klabu hiyo, ila mipango ambayo imewekwa na viongozi wa The Blues ilimsukuma nje na kushindwa kusaini mkataba mpya.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 36 amesisitiza kwamba kuondoka kwake Chelsea kulitokana na mkataba kufikia kikomo na hakuna shida yoyote iliyojitokeza kati yake na viongozi wa ngazi za juu.

‘Nilikuwa tayari kubaki na kuendelea kuitumikia Chelsea kwa kipindi kingene, endapo viongozi wangenionyesha utayari wao wa kufanya hivyo, ila ilikua tofauti na ilinithibitishia sina changu Stamford Bridge.” Amesema Lampard.

Hata hivyo madai hayo ya Lampard yanakinzana na maelezo yaliyotolewa na meneja wa Chelsea Jose Mourinho mwezi uliopita ambapo alisema uongozi wa The Blues ulikuwa tayari umeshakubali kumpa mkataba mpya kiungo huyo sambamba na beki wa pembeni Ashley Cole lakini kwa wote wawili walipuuza suala hilo na kuamua kuondoka.

Frank Lampard ameondoka Chelsea baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 13 mfululizo, ambapo kama itakumbukwa vyema mwaka 2001 alisajiliwa na The Blues akitokea West Ham Utd kwa ada ya uhamisho wa paund million 11.

0 comments:

Post a Comment