Apr 8, 2015

WASTARA AANDIKA HISTORIA...Shoo ya Ali Kiba Dar Live


WASTARA AANDIKA HISTORIA...Shoo ya Ali Kiba Dar Live


Waandishi Wetu
AJABU! Staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma usiku wa kuamkia Jumatatu aliandika historia ya aina yake ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani wa Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, Dar kwa kuonesha shoo ya nguvu jukwaani hivyo kuwafanya mashabiki kibao waliohudhuria ukumbini hapo kupigwa butwaa wasiamini kama ni yeye.
Staa wa filamu za Kibongo, Wastara Juma akicheza kwa hisia.Katika shoo hiyo ya Sikukuu ya Pasaka iliyotambulika kwa jina la Mwana Dar Live, wasanii, Msaga Sumu, Ali Kiba na Isha Mashauzi walitumbuiza, lakini Wastara alihudhuria maalum kwa ajili ya Ali Kiba.


ATINGA NA TIMU KIBA
Wakati jukwaani akiimba msanii wa muziki wa Vigodoro, Msaga Sumu, kundi kubwa lililojulikana kama ‘Team Kiba’ likiwa na watu zaidi ya kumi lilitinga ukumbini hapo likiongozwa na Ali Kiba mwenyewe huku Wastara akiwa miongoni mwao.


AJIWEKA KARIBU NA DADA KIBA
Katika hali ya kushangaza, punde baada ya kundi hilo kutinga ukumbini hapo, Ali Kiba alipanda jukwaani na kumuacha Wastara akiwa sanjari na dada wa Kiba aitwaye Zabibu Kiba huku muda wote akionekana kucheka na kurusha mikono kwa shangwe.

Kudhihirisha kuwa amekuja kama Team Kiba, staa huyo alionekana kukongwa na nyimbo zilizokuwa zikiimbwa na Kiba kiasi cha kuanza kuserebuka hadharani huku Zabibu akimpa sapoti kwa kuibiaibia kiaina.
Kitendo cha kuendelea kuserebuka nyuma ya jukwaa kiliwashangaza baadhi ya watu huku wengine wakiwa hawaamini kama ni Wastara wanayemjua wao.


“Jamani kweli huyu ni Wastara tunayemjua au? Mh! Mimi sijawahi kumwona akisakata muziki kama hivi. Ama kweli Dar Live ndiyo kiwanja cha burudani, ingekuwa viwanja vingine sidhani kama angejiachia,” ilisikika sauti ya shabiki mmoja wa muziki baada ya kukosa uzalendo kwa kumuangalia Wastara.


WATU WAPIGWA BUTWAA
Baada ya kusakata mauno nyuma ya jukwaa kumnogea na kusababisha kuzua minong’ono ya hapa na pale, mdada mmoja alionekana kuvutiwa na staa huyo na kuamua kumshika mkono kwa kumtaka apande jukwaani ili akawadhihirishie mashabiki wote kuwa, anayaweza kama si kuyamudu!
Awali, Wastara alionekana kukataa katakata na kugeuza kichwa huku na kule kwa aibu lakini dakika kama tatu mbele, ghafla aliibukia jukwaani ambapo Ali Kiba pamoja na mdogo wake, Abdu Kiba walikuwa wakiimba pamoja wimbo wa Chekecha Cheketua na kuwafanya mashabiki kupigwa butwaa.


ATUMIA ZAIDI YA DAKIKA TATU
Wastara aliyevaa suruali nyesi na juu kitop cha jinzi, akiwa jukwaani hapo, bila kupepesa macho alianza kwa kuwanyooshea mkono mashabiki wake kisha akawageuzia mgongo na kuanza kuyakata mauno kwa staili ya Chekecha Cheketua huku baadhi ya mashabiki hao wakiwa hawaamini kwa kile alichokuwa akikifanya, wengine walitamani kupanda jukwani wakajirushe naye.
Pale jukwaani, Wastara alitumia zaidi ya dakika tatu kiasi cha kuwafanya Ali na Abdu kushusha vipaza sauti vyao na kumuangalia staa huyo akiwafundisha mashabiki staili ya wimbo huo wa Cheketua.
Hadi anaondoka kwenye jukwaa hilo la kisasa, mashabiki walikuwa wakimshangilia staa huyo wengine wakisema kumbe ni fundi wa kucheketua!
“Loo! Wastara bwana! Leo amenifanya nimpende zaidi, kumbe anayaweza, huwezi amini kabisa. Ama kweli Mungu kila mtu kampa kipawa chake,” alisema shabiki mmoja huku macho yake yakimsindikiza Wastara wakati anaondoka.


TUJIKUMBUSHE
Wastara alifunga ndoa Juni 6. 2009 na msanii mwenzake, Juma Kilowoko ‘Sajuki’ (sasa marehemu). Wakiwa wachumba wawili hao walipata ajali mbaya ya bodaboda maeneo ya Tabata jijini Dar ambapo Wastara alivunjika mguu na baadaye kukatwa kabisa hivyo kumfanya awekewe mguu wa bandia.
Katika kipindi chote hicho na hasa baada ya kifo cha Sajuki, Wastara amekuwa akiishi katika mazingira ya kidini na hakuwahi kuonekana akicheza muziki hadharani kama vile, hivyo alichokifanya usiku huo kwake ni kuandika historia mpya ya maisha yake ya ustaa.Kwa kilichotokea kwenye upande wa burudani usiku huo, nenda Ukurasa wa 8&9.Imeandaliwa na Andrew Carlos, Mayasa Mariwata, Deogratius Mongela na Shani Ramadhani.CHANZO: RISASI MCHANGANYIKO-GPL

0 comments:

Post a Comment